Success, we'll get back to you
Back to news

NIC, Coop Bank wasaini Mkataba wa Makubaliano Kukuza wigo wa sekta ya bima.

SHARE

Katika hatua ya kuongeza ushirikishwaji wa kifedha na kupanua wigo wa huduma za bima kote nchini, Benki ya Ushirika (Coop Bank Tanzania) imesaini Mkataba wa Makubaliano (MOU) na Shirika la Bima la Taifa (NIC) wa miaka mitatu utakaoiwezesha benki yetu kusambaza bidhaa mbalimbali za bima za NIC kupitia mtandao wa matawi ya benki yetu.


Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika Makao Makuu ya Coop Bank jijini Dodoma, ikiashiria hatua kubwa katika kuwezesha wananchi kote nchini kupata huduma za bima.


Ushirikiano huo mpya utawezesha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali za bima za jumla na za maisha zikiwemo bima za magari, moto, afya kupitia matawi yetu ya Coop Bank.


Akizungumza wakati wa hafla fupi ya utiaji saini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank Godfrey Ng’urah, aliupongeza ushirikiano huo huku akisisitiza kuwa makubaliano hayo ni nyenzo madhubuti katika kukuza uchumi jumuishi wa Watanzania kwa ujumla.


"Mkataba huu na NIC ni zaidi ya biashara kwetu. Sisi kama Coop Bank tunaamini kuwa mkataba huu utakuwa chachu ya kutekeleza dhamira yetu ya kulinda na kuwezesha maisha ya wateja wetu na watanzania kwa jumla. Kwa kuunganisha bima katika huduma za matawi yetu, tutakuwa tumewarahisishia Watanzania, hasa wa vijijini, kulinda vitu muhimu zaidi kwao,” alisema.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Abdi Mkeyenge wakati wa hafla hiyo alisisitiza dhamira ya shirika hilo kuendelea kusogeza huduma za bima karibu na wananchi.


Utekelezaji wa mkataba huo unaanza rasmi leo na bidhaa mbalimbali za bima za NIC sasa zitapatikana kwenye mtandao wa matawi ya Coop Bank yaliyopo Dodoma, Moshi, Tandahimba na Tabora.

@2025

National Insurance Corporation of Tanzania Limited