Kampeni ya kutoa elimu na huduma za bima mtaani ijulikanayo kama NIC Kitaa imezinduliwa rasmi mkoani Iringa ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo wanayoishi na kufanya shughuli zao.
NIC limejipanga kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa bima za maisha na mali, sambamba na kuwawezesha kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya majanga yanayoweza kutokea bila kutarajiwa.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa NIC, Karimu Meshack, alisema dhamira kuu ya kampeni hiyo ni kusogeza huduma za bima karibu na wananchi kwa kuwapa elimu ya moja kwa moja na kujibu maswali yao papo kwa hapo. Meshack alisema kwamba soko la bima nchini bado ni dogo—likiwa asilimia 2.8 pekee—na moja ya sababu ni wananchi kutofikiwa moja kwa moja na watendaji wa sekta hiyo. “Usipokuja mtaani unapunguza kasi ya wananchi kujua umuhimu wa bima. Sisi kama shirika kongwe lazima tuoneshe njia. Tumeshuhudia wananchi wanajenga nyumba kwa miaka mingi lakini zinapoteketea wanakosa fidia,” alisema.
Alibainisha kuwa kampeni hiyo ambayo pia imekwishafanyika katika baadhi ya mikoa nchini, safari hii imeelekezwa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ukiwemo mkoa wa Iringa na Njombe. Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesema:
“Bima ni usalama wa maisha na mali zetu.” Aliunga mkono kampeni hiyo akibainisha kuwa serikali inaendelea kusukuma agenda ya elimu ya bima kwa wananchi kupitia taasisi zake.
“Bima inatupa usalama wa mali na maisha yetu. Tunajipa uhakika pale mali zinapopotea au tunapopata madhara. Ni muhimu sana taasisi kama NIC kuwafuata wananchi walipo kwenye shughuli zao, masoko na mitaani hasa kwa sababu wengi hawapati muda wa kufuatilia vyombo vya habari,” alisema.
Kheri James alisema wiki nzima ya kampeni mkoani Iringa itatoa fursa ya kutosha kwa wananchi kupata elimu kuhusu namna bima inavyoweza kuwa kinga madhubuti dhidi ya majanga na hasara.
Meneja wa NIC wa mikoa ya Iringa na Njombe, Paul Mkumbo, ameeleza kwa kina aina za bima zinazotolewa na NIC, ikiwemo: Bima ya Mali ambayo kazi yake ni kulinda nyumba, biashara, majengo ya taasisi na mali nyingine dhidi ya moto, wizi, mafuriko na majanga mengine.
Nyingine ni bima ya maisha: ambayo hutoa msaada wa kifedha kwa familia endapo mhusika atafariki au kupata ulemavu wa kudumu. Alitaja bima nyingine kuwa ni zile zinazolinda mkulima, mfanyabiashara au mfanyakazi binafsi dhidi ya ajali au gharama za matibabu, bima ya usafiri nabima za kibiashara kwa kampuni, viwanda, mashirika na biashara ndogo ndogo zenye uhitaji wa kulinda biashara na vifaa vyake.
Amesema hudumu hizo zinapatikana kwa gharama rafiki, na kampeni ya NIC Kitaa inalenga kuhakikisha wananchi wanaelewa kile wanachokilipia na faida wanazopata.