Success, we'll get back to you
Back to news

NIC Yaimarisha Ushirikiano na Wadau wa Sekta ya Fedha

SHARE

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge, ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha pamoja na wateja wakubwa wa bima.


Katika ziara hiyo, Bw. Mkeyenge ametembelea taasisi muhimu zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na Wakala wa Bima wa Charaj Insurance Agency, akisisitiza dhamira ya NIC ya kuendelea kutoa huduma bora na zenye ubunifu kwa wateja wake kote nchini.


“Tunaendelea kuhakikisha mteja wetu anapata huduma kwa kiwango cha juu, Mteja kwanza. NIC itaendelea kuboresha huduma zake na kuimarisha ushirikiano na wadau wote wa sekta ya bima,” amesema Bw. Mkeyenge.


Bw. Mkeyenge ameongeza kuwa mafanikio ya NIC katika sekta ya bima ni kielelezo cha utekelezaji wa vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, vinavyolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani wa kikanda na kimataifa.


Kupitia ripoti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ya mwaka 2024, NIC imeendelea kuongoza katika maeneo mengi ya soko la bima nchini, jambo linalodhihirisha uwezo wa Shirika katika kuimarisha mifumo ya kifedha na kulinda rasilimali za taifa.


“Tumeendelea kufanya vizuri kwenye sekta ya bima; kwenye ripoti ya TIRA ya 2024 iliyotolewa hivi karibuni, NIC inaongoza katika maeneo mengi ya soko. Haya mafanikio ni matokeo ya ushirikiano wenu mzuri; nawashukuru sana,” aliongeza Bw. Mkeyenge.


Shirika linaahidi kuimarisha ubunifu, kuongeza ufanisi wa huduma, na kujenga ushirikiano thabiti na sekta binafsi na taasisi za umma, ili kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na mfumo wa bima unaochochea ustawi wa kijamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Ziara ya kikazi ya Mkurugenzi Mtendaji inaendelea katika mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.

@2025

National Insurance Corporation of Tanzania Limited