DAR ES SALAAM. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imelitaka Shirika la Bima la Taifa (NIC) kutumia fursa za biashara zilizopo nchini kuimarisha uwezo wake wa kushindana ndani na nje ya Tanzania, sambamba na malengo ya Dira 2050.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika ofisi za NIC jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Elibariki Kingu, amesema miradi ya kimkakati yenye thamani ya takribani Sh trilioni 172.5 inayotekelezwa nchini inatoa fursa kubwa kwa shirika hilo kupanua biashara yake.
Ametaja fursa hizo kuwa katika miradi ya gesi asilia, Liganga na Mchuchuma, Bagamoyo Eco Maritime City, pamoja na uwekezaji katika viwanda, kilimo na madini.
Mhe. Kingu ameitaka NIC kuwasilisha mikakati ya kushiriki katika miradi hiyo na kubainisha vikwazo vinavyoathiri azma yake ya kuongeza sehemu ya soko la bima hadi angalau asilimia 30.
Maelekezo hayo yanaendana na nguzo ya Dira 2050 ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, inayosisitiza kuimarisha biashara za ndani, kuvutia uwekezaji na kukuza ushiriki katika masoko ya kikanda na kimataifa. Kwa NIC, kuhudumia miradi mikubwa kunaweza kuongeza mapato, kukuza utaalamu na kuimarisha uwezo wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya ushindani wa kimataifa.
Huduma za bima katika miradi hiyo pia zina nafasi muhimu katika kulinda mitaji, mali na shughuli za uzalishaji dhidi ya hasara zinazolindwa na bima, hivyo kusaidia uwekezaji kuendelea na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Pamoja na maelekezo hayo, Mhe. Kingu amelipongeza shirika hilo kwa kuimarika kwa viashiria vyake vya kifedha, hususan kupungua kwa uwiano wa madai ya bima.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amesema Serikali inaendelea kuwa na imani na NIC kama taasisi muhimu katika sekta ya bima nchini.
Amesema hatua ya Serikali kuliondoa shirika hilo katika orodha ya taasisi zilizokuwa zikizingatiwa kwa ajili ya ubinafsishaji ni miongoni mwa vielelezo vya imani hiyo.
Mauki ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano, thamani ya mali za NIC imeongezeka kutoka Sh bilioni 350 hadi karibu Sh bilioni 600.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Abdulkarim Kisuguru, amesema sehemu ya Shirika hilo katika soko la bima ya jumla imeongezeka kutoka asilimia 9.45 mwaka 2023/24 hadi asilimia 10.23 mwaka 2024/25.
Amesema mkakati wa NIC wa miaka mitano unalenga kuimarisha mtaji, kuongeza mapato endelevu na kupanua maeneo ya uwekezaji na utoaji wa huduma.
Katika maoni yao, Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati wameitaka NIC kupanua huduma kwa wakulima, wajasiriamali na wananchi wenye kipato cha chini. Pia wamehimiza kuboreshwa kwa huduma za bima ya maisha na kuongezwa kwa ufanisi katika ulipaji wa madai.
Kupanua huduma kwa makundi hayo ni utekelezaji na msisitizo wa Dira 2050 wa kujenga uchumi unaowashirikisha wananchi wengi zaidi, pamoja na nguzo ya uwezo wa watu na maendeleo ya jamii. Bima inaweza kusaidia familia na wajasiriamali kulinda mali na vyanzo vya kipato, na kurejea katika shughuli zao baada ya kupata hasara zinazolindwa na bima.
Wajumbe pia wamehimiza shirika hilo kupunguza urasimu, kutafuta fursa zaidi za biashara ndani na nje ya Tanzania na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi walio katika mikataba kwa muda mrefu.
Aidha, wameitaka NIC kuhakikisha manufaa ya shughuli zake za uwajibikaji kwa jamii yanawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamati imesisitiza kuwa NIC inapaswa kutumia mafanikio iliyoyapata kama msingi wa kuongeza ushindani, kupanua wigo wa huduma na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa taifa.